• Email za Serikali |
    • Malalamiko |
    • Maswali ya Mara kwa Mara |
    • Mawasiliano |
    • Mifumo |
Simanjiro District Council
Simanjiro District Council

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro

  • Mwanzo
  • About us
    • Historia
    • Dira na Dhima
    • Maadili ya Msingi
  • Administration
    • Muundo wa Halmashauri
    • Sehemu
      • Infastructure,Rural and Urban Development
        • Works
        • Roads
        • Rural & Urban Development
      • Health,Social Walfare & Nutrition Services
        • Health Services
        • Nutrition Services
        • Social Walfare
      • Industry ,Trade and Investment
        • Industry Development & Investment
        • Trade & Marketing
      • Pre-Primary & PPrimary Education
        • Academics
        • Special Needs Education
        • Adult & Non Formal Education
      • Seconadry Education
        • Academics
        • Statistics & Logistics
        • Special Needs
        • Adult & Non Formal Education
      • Community Development
        • Cross-Cutting Issues Cordination
        • Ngos's & Cbos's Coordination
      • Agriculture,Livestock and Fisheries
        • Agriculture
        • Livestock
        • Fisheries
      • Administration & Human Resources Management
        • Human Resource Management
        • Utawala
      • Planning and Coordination
        • Planning and Budgeting
        • Monitoring and Evaluation
      • LGA'S LAND ADMINISTRATION OFFICE-Ministry of Land ,Housing and Humman Settlement
    • Vitengo
      • Sports,Culture & Arts
      • ICT Unit
      • Government Communication Unit
      • Waste Management & Sanitation Unit
      • Legal Services Unit
      • Internal Audit Unit
      • Procurement Management Unit
      • Natural Resources & Environment Unit
      • Finance & Accounts Unit
  • Fursa za Uwekezaji
    • Madini
    • Utalii
    • Kilimo
    • Ufugaji
  • Huduma zetu
    • Utoaji wa Leseni za Biashara
    • Utoaji wa Lesseni za Vileo
    • Utoaji wa Vibali vya Ujenzi
    • Utoaji wa Leseni Za Makazi
    • Utoaji wa Mikopo ya Asilimia Kumi(10%)
    • Upimaji wa Ardhi
    • Usajili wa Vikundi vya Kijamii
    • Uandikishaji wa Bima ya Afya ya Jamii(iCHF)
    • Utoaji wa Vitambulisho vya Wajasiriamali Wadogo
    • Kulipia Tozo Za Halmashauri
  • Madiwani
    • Orodha ya Madiwani
    • Kamati za Huduma za Halmashauri
      • Kamati ya Kudhibiti ukimwi
      • Kamati ya Huduma za Jamii
      • Kamati ya Uchumi,Ujenzi na Mazingira
      • Kamati ya Maadili
      • Kamati ya Fedha,Uongozi na Mipango
    • Suku ya Kumwona Mwenyekiti wa Halmashauri
  • Miradi
    • Miradi iliyoidhinishwa
    • Miradi inayoendelea
    • Miradi iliyokamilika
  • Machapisho
    • Fomu za Maombi
    • Report
    • Vipeperushi
    • Miongozo Mbalimbali
    • By Laws
    • Mpango Mkakati
  • Kituo cha habari
    • Taarifa kwa vyombo vya habari
    • Hotuba

SHERIA ZINAZOSIMAMIA UTUMISHI WA UMMA ,HAKI NA WAJIBU WA MTUMISHI WA UMMA

Friday 9th, May 2025
@SIMANJIRO DC


SHERIA ZINAZOSIMAMIA UTUMISHI WA UMMA, HAKI NA WAJIBU WA MTUMISHI WA UMMA


2.1 Utangulizi

 Katika mada hii utajifunza haki na wajibu wako katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mada hii itakuwezesha kutambua sheria zinazosimamia Utumishi wa Umma, haki na wajibu wako, na makosa na adhabu zinazotokana na ukiukwaji wa misingi ya mienendo na utendaji kazi katika Utumishi wa Umma.

Malengo Mahsusi


Baada ya kujifunza mada hii, utaweza:-
  1. Kuainisha sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma,
  2. Kuzingatia sheria za Utumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu ya kazi,
  3. Kuanisha haki na wajibu wa Mtumishi wa Umma,
  4. Kuainisha makosa na adhabu mbalimbali zilizoko kwenye Utumishi wa Umma.

 

2.2 Sheria za Utumishi wa Umma

Tambua kwamba uendeshaji wa Utumishi wa Umma, unapaswa kuzingatia sheria mbalimbali zilizoko kwenye Utumishi wa Umma ili kuwa na utumishi unaotoa haki bila upendeleo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Aidha zipo Sera, Sheria, na Kanuni zinazosimamia Utumishi wa Umma.

2.2.1 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya 2

Kwa mujibu wa ibara ya 36 (1-2) ya Katiba, Rais ana mamlaka ya kuanzisha, kuteua na kufuta nafasi za madaraka katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Pia, ibara 36(3) ya Katiba imempatia mamlaka Rais kuanzisha Tume ya Utumishi wa Umma yenye mamlaka ya kusimamia Utumishi wa Umma na mamlaka ya rufaa ya watumishi wa umma ambao hawateuliwi na Rais. Rejea kielelezo Na 2.1.


Kielelezo Namba 2.1: Kinaonesha ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mwisho ibara ya 36(4) ya Katiba inampatia mamlaka Rais kuchukua hatua za kudhibiti nidhamu ya watumishi na utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

2.2.2 Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, 1999

Tamko namba 1 hadi 7 la Sera husika linatoa tafsiri ya Utumishi wa Umma, misingi na malengo ya Utumishi wa Umma na maadili ya msingi ya uwepo wa Utumishi wa Umma. Pia, sera husika inaweka sifa za msingi za kujiunga kwenye Utumishi wa Umma, uwepo wa mipango ya watumishi, ajira na uteuzi. Vile vile uwepo wa mikataba ya ajira, upandishwaji wa madaraja, usimamizi wa tathmini ya utendaji kazi, mafunzo kazini, mahusiano kazini, mwenendo na nidhamu kazini, na majukumu ya msingi ya wadau wa Utumishi wa Umma.

2.2.3 Sheria ya Utumishi wa Umma sura ya 298, 2019

Kifungu cha 4-8 cha Sheria hii kinazungumzia usimamizi wa Utumishi wa Umma. Kifungu cha 9-20 cha sheria husika kinaanzisha Tume ya Utumishi wa Umma pamoja na masuala yanayohusiana na tume hiyo.  Pia, kifungu cha 21-25 kinatoa ufafanuzi wa mamlaka ya Rais katika usimamizi wa Utumishi wa Umma. Aidha, kifungu cha 26-28 kinazungumzia masuala ya mafao ya hitimisho la kazi. Vilevile, kifungu cha 29-36 cha sheria kinatoa ufafanuzi wa masuala ya kiujumla ya kiutumishi kama kuumia kazini kwa watumishi wasio maafisa (operational services).

2.2.4 Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, 2004

Sheria hii imetungwa ili kuweka masharti ya kazi, vigezo vya msingi vya ajira, muundo kwa ajili ya majadiliano ya pamoja, kuweka mifumo ya kuzuia na kutatua migogoro na mambo mengine yanayofanana na hayo. Sheria hii inatumika kwa wafanyakazi wote ikiwa ni pamoja na wale wa sekta binafsi.

2.2.5 Sheria ya Taasisi za Kazi, 2004

Sheria hii imetungwa kwa ajili ya kuanzisha Taasisi za kutolea maamuzi mbalimbali ya kiutumishi na ajira kama vile Kamisheni ya Usuluhishi na Uamuzi ikiainisha mamlaka na wajibu wake na mambo mengine yanayofanana na hayo.

2.2.6 Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009

Kanuni hizi zimebeba masharti ya ujumla katika Utumishi wa Umma na zimetengenezwa chini ya kifungu cha 35 (5) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 (2002). Kanuni hizi ni toleo la tatu na zilianza kutumika rasmi tarehe 1 Julai, 2009.

Kanuni hizi zinatoa ufafanuzi wa masuala mengi ya kiutumishi kama vile ajira, uteuzi, nidhamu, kuthibitisha kazini watumishi, likizo, matibabu, mafunzo, mitihani, posho mbalimbali, mikopo ya watumishi, nyumba na samani na uendeshaji wa jumla wa Utumishi wa Umma.

2.2.7 Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003

Kanuni hizi zimetungwa chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma, 2002. Kanuni zinaeleza masuala ya msingi yanayohusu ajira au uteuzi wa watumishi wa umma, kuthibitishwa kazini; tathmini ya utendaji kazi; kupandishwa cheo; kusitishwa kwa ajira; nidhamu; rufaa; kanuni za maadili za watumishi wa umma; na mafao ya kustaafu. Pia, kanuni zinaeleza majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma.

Angalizo


  1. Licha ya uwepo wa sheria zilizotajwa hapo juu, unatakiwa kuzisoma na kuzifahamu sheria nyingine zinazohusu maeneo maalum kama kuumia kazini, hitimisho la kazi, Sheria ya Usalama wa Taifa, Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria ya Ulipwaji wa Hasara na Fidia alizozisababisha mtumishi kwa serikali.

 

2.3 Haki na Wajibu wa Mtumishi wa Umma

Mtumishi wa Umma una wajibu wa kutumia elimu, ujuzi na bidii katika kutoa huduma bora kwa wananchi. Kadhalika una haki na stahiki mbalimbali unazopaswa kuzipata kutoka kwa mwajiri wako kama ifuatavyo:- 

2.3.1 Kupewa Mkataba wa Kazi (Barua ya Ajira)

Mtumishi wa Umma una haki ya kupewa barua ya ajira inayoonesha jina lako, anuani yako, tarehe ya ajira, aina ya ajira, cheo, ngazi ya mshahara, kiwango cha mshahara na masharti mengine ya ajira yako [Rejea Kanuni D.32 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009].

2.3.2 Posho ya Kujikimu

Unapoajiriwa kwa mara ya kwanza unastahili kulipwa posho ya kujikimu ya siku 7 kwa ajili yako,. (Rejea Kanuni ya L. 6. Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2011). Aidha, unastahili kupata posho ya njiani kwa safari inayozidi masaa sita (6). Posho hii hulipwa kwa kiwango cha nusu ya posho ya kujikimu ya siku moja [Rejea Kanuni L. 2(3) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009].

2.3.3 Kuthibitishwa Kazini

Una haki ya kuthibitishwa kazini baada ya kipindi cha majaribio kisichozidi miezi kumi na mbili (12) chenye lengo la kupima tabia na utendaji wako wa kazi. Miezi mitatu (3) kabla ya muda wa majaribio kuisha, msimamizi wako wa kazi anapaswa kuamua kama:

  • Uthibitishwe kazini, au
  • Uongezewe muda wa majaribio, au
  • Ajira yako isitishwe.

Rejea Kanuni ya 14 (1) na (2) (a), (b) na (c) ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003 na Kanuni D.40 na D.43 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009.

 



 

2.3.4 Likizo Maalum (Ruhusa)

Una haki ya kupewa ruhusa isiyozidi siku kumi na nne (14) kwa mwaka ili kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali ambayo hayaepukiki kama vile msiba wa ndugu wa karibu ambao ni pamoja na baba, mama, mwenza na mtoto, kushiriki vikao vya vyama vya wafanyakazi, michezo, kuuguza, kufunga ndoa n.k. Iwapo utaomba ruhusa zaidi ya muda huo basi siku zitakazozidi siku kumi na nne (14) ni lazima zikatwe kutoka kwenye likizo yako ya mwaka.

Ni kosa kuomba ruhusa kufanya shughuli binafsi kama kulima, biashara, kufuga, kueneza dini au kufanya siasa kwani ni wizi wa muda wa serikali (Rejea Kanuni H.14 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, 2009).

2.3.5 Likizo ya Mwaka

Baada ya kupita miezi nane (8) tangu ulipoajiriwa unastahili kwenda likizo ya mwaka ya siku ishirini na nane (28) ikijumuisha siku za Jumamosi na Jumapili na siku za sikukuu. Katika likizo hiyo, wewe, mwenza wako na watoto au wategemezi wasiozidi wanne mtakuwa na haki ya kulipwa nauli kwenda na kurudi kwenye makazi yako ya kudumu mara moja ndani ya kipindi cha miaka miwili cha mzunguko wako wa likizo [Rejea Kanuni H.1 (1), (2) na (3) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009 na Kanuni ya 97 (1) na (2) ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003].

Iwapo mwajiri atazuia likizo yako ya mwaka utastahili kulipwa mshahara wa mwezi mmoja bila ya makato kama fidia [Rejea Kanuni ya 97(3) ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003].

2.3.6  Likizo ya Uzazi kwa Mwanamke

Ikiwa wewe ni mwanamke unastahili likizo ya siku themanini na nne (84) au siku tisini na nane (98) (kama utajifungua watoto mapacha) ikiwa ni likizo ya uzazi mara moja ndani ya kipindi cha miaka mitatu. Likizo hii haitaingiliana na likizo yako ya kawaida ya mwaka na iwapo ujauzito utaharibika au mtoto kufariki ndani ya miezi kumi na mbili (12) baada ya kujifungua, utastahili haki ya likizo ya uzazi katika ujauzito utakaofuata bila kujali masharti ya miaka mitatu [Rejea Kanuni H.12 (1-7) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009].

Aidha, kama utajifungua kabla ya kutimiza miaka mitatu baada ya kujifungua utastahili wiki 6 ambazo ni sawa na siku (42) siku hizi zitakakatwa/hazitakatwa katika likizo yako ijayo kulingana na mzunguko wako wa likizo. 

2.3.7 Likizo ya Uzazi kwa Mwanaume

Ikiwa wewe ni mwanaume unastahili likizo ya uzazi ya anaglau siku tatu (3) mara moja ndani ya kipindi cha miaka mitatu (3) iwapo mke wako atakuwa amejifungua. Likizo hii inapaswa kuchukuliwa ndani ya siku 7 tangu mke wako alipojifungua na haitaingiliana na likizo ya mwaka [Rejea Kanuni ya H.13 (a) na (b) ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, 2009].

2.3.8 Likizo Bila Malipo

Likizo hii hutolewa kwa muda usiozidi miaka mitatu (3) ili kukuwezesha kujiunga na mashirika ya umma, programu za kimataifa na mashirika ya kimataifa/ kitaifa yenye uhusiano na serikali. Ili kupata likizo hii ni sharti uwe umethibitishwa kazini na hauna mashauri ya kinidhamu. Maombi ya likizo hii hupelekwa kwa Katibu Mkuu Utumishi kupitia kwa mwajiri wako. Aidha, hupaswi kulipwa mshahara, kupandishwa daraja na stahiki zako zote zitasimamishwa katika kipindi chote cha likizo hii [Rejea Kanuni ya 99 (1) na (2), ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003, na Kanuni H.19 (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009].

2.3.9 Likizo ya Ugonjwa

Likizo hii hutolewa kwa mtumishi mgonjwa baada ya kupata mapendekezo ya daktari yakithibitisha kwamba unapaswa kupumzika. Hutolewa kwa muda wa mwaka mmoja kwa utaratibu wa miezi sita (6) ya mwanzo, ambapo utapokea mshahara kamili na miezi sita ya mwisho utapokea nusu mshahara. Endapo hutakuwa umepona katika kipindi cha mwaka mmoja  utastaafishwa kazi kwa ugonjwa [Rejea Kanuni ya 100 (1-2) ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003].

2.3.10 Ruhusa ya Masomo

Ruhusa hii hutolewa baada ya mwajiriwa mpya kufanya kazi zaidi ya miaka miwili. Unaweza kuruhusiwa kwenda masomoni baada ya kuomba kuwekwa kwenye mpango wa mafunzo wa Taasisi.  Utaweza pia kuomba kugharamiwa na mwajiri au kujigharamia mwenyewe au kuomba ufadhili kupitia Bodi ya Mikopo n.k. Kwa kuwa nia ya masomo ni kukuendeleza kitaaluma, ni vema ukajiendeleza katika fani unayofanyia kazi (proffessional carrier development) [Rejea Kanuni ya G.7(1)(a-j) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009].kwa mujibu wa  Mwongozo wa Uendeshaji wa Mafunzo kwa Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Wa mwaka 2008

2.3.11 Ruhusa Kwenda Nje ya Kituo cha Kazi

Huruhusiwi kutoka nje ya kituo chako cha kazi wakati wa saa za kazi bila ya ruhusa ya msimamizi wako. Pia, huruhusiwi kutoka nje ya kituo chako cha kazi kwenda nje ya mkoa wako bila ya ruhusa ya maandishi toka kwa mwajiri. Unapaswa kuomba ruhusa ya kwenda nje ya mkoa hata kama utasafiri siku za Jumamosi, Jumapili na siku za Sikukuu. Pia, huruhusiwi kusafiri nje ya nchi bila ya kibali cha Katibu Mkuu Kiongozi [Rejea Kanuni ya F.17(1-2) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009].

2.3.12 Likizo ya Kustaafu

Utakapokaribia kustaafu utastahili kupewa likizo ya siku ishirini na nane (28) ili kukuwezesha kujiandaa kabla hujastaafu (Rejea Kanuni ya 102 ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003).

2.3.13 Kupanda Madaraja ya Utumishi wa Umma

Kwa kuzingatia sifa za kimuundo, utendaji wa kazi, nidhamu kazini na uwepo wa bajeti ya mishahara mipya iliyotengwa na mwajiri, unastahili kupandishwa cheo (daraja) baada ya miaka mitatu

 tangu kuthibitishwa kazini au kila baada ya miaka mitatu (3) unapopanda kwa mara ya pili na kuendelea (Rejea Kanuni ya D.51 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, 2009 na Waraka wa Katibu Mkuu Kumbukumbu CAC.45/257/01/E/83 wa tarehe 09 Septemba, 2013). Aidha, muda wa miaka mitatu (3) katika kupanda utategemea pia maagizo na maelekezo mbalimbali kutoka Ofisi ya Rais UTUMISHI katika kipindi cha utekelezaji wa IKAMA.

2.3.14 Matibabu

Unastahili kugharamiwa na mwajiri wako matibabu ambayo hayagharamiwi na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Unastahili kulipwa posho ya kujikimu na nauli kwenda kutibiwa nje ya kituo chako cha kazi, endapo utapewa rufaa na daktari [Rejea Kanuni 1 (1-2) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009]. Aidha, ukilazwa hustashili kulipwa posho ya kujikimu,.

2.3.15 Uhamisho

Unaweza kuhamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kingine na kustahili kulipwa malipo yafuatayo:

  • Posho ya kijikimu kwa siku 14 kwako, mwenza wako na nusu ya kiwango kwa watoto/wategemezi wako wasiozidi wanne.
  • Posho ya usumbufu kwa kiwango cha asilimia kumi (10%) ya mshahara wako wa mwaka mzima
  • Gharama ya kusafirisha mizigo kati ya tani 1.5 hadi tani 3 (kutegemea kiwango cha ngazi ya mshahara wa mtumishi)
  • Posho ya kujikimu ukilala njiani
  • Nauli

Endapo utaomba kuhama kwa sababu zako mwenyewe na umeishi zaidi ya miaka mtano (5) katika kituo chako cha kazi, au katika mazingira maalum mtumishi anapokaribia kustaafu na amefanya kazi nje ya Mkoa wake kwa muda wa miaka 10 mfululizo au zaidi, basi utastahili malipo husika kama mwajiri anao uwezo [Rejea Kanuni ya 107(1-5) ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003 Kanuni J.4  na L.8  ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009].

2.3.16 Fidia ya Kuumia au Kufa Ukiwa Kazini

Endapo utaumia  au kufariki ukiwa kazini, utastahili kulipwa fidia kupitia Mfuko wa Fidia wa Watumishi (Rejea Kanuni  ya 110 ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003).

2.3.17 Mikopo Mbalimbali

Una haki ya kukopa kwenye taasisi za kifedha/mikopo kwa makato ambayo kwa mwezi hayatazidi 2/3 ya mshahara wako. Hivyo basi, 1/3 ya mshahara wako ni lazima ibaki ili kukuwezesha kumudu maisha na kuondokana na mzigo wa madeni ili utekeleze majukumu yako ya kazi kwa ufanisi (Rejea Kanuni F.12 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009).ikisomwa pamoja na Ufafanuzi Kuhusu  Utaratibu wa Kusiamamia Mikopo inayotolewa kwa Watumishi wa Umma na Serikali au Taasisi za Fedha,uliotolewa na Ofisi ya Rais Utumishi wa mwaka 2013.

2.3.18 Kushiriki Katika Shughuli za Vyama vya Wafanyakazi

Una haki ya kujiunga na kuwa kiongozi wa chama cha wafanyakazi kama vile TALGWU, TUGHE, CWT na CHAKAMWATA. Ni muhimu katika ushiriki huo, ukazingatia sheria na kujiepusha na migogoro na migomo isiyo ya kisheria (Rejea F.22 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009).

2.3.19 Posho ya Masaa ya Ziada

Iwapo utapata kibali cha kufanya kazi zaidi ya muda wa kawaida wa masaa ya kazi na umeajiriwa ukiwa mtumishi asiye wa zamu kama vile watumishi wa kada za afya, walinzi n.k., utastahili kulipwa posho ya masaa ya ziada kwa kiwango kilichowekwa na serikali (Rejea Kanuni ya L.21-22 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009).

2.3.20 Posho ya Kukaimu Madaraka

Iwapo utateuliwa kukaimu cheo cha madaraka kama vile Ukuu wa Idara au Ukurugenzi kwa zaidi mwezi mmoja (1) utastahili kulipwa posho ya kukaimu madaraka. Kiwango hicho ni tofauti ya mshahara wa cheo unachokaimu na mshahara wako wa cheo cha sasa (Rejea Kanuni ya L.15-18 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009) ikisomwa kwa pamoja na  waraka wa Utumishi wa Umma Na.3,2018 Kuhusu Utaratibu wa Kukaimu Nafasi ya Uongozi. Pia, endapo mtumishi hajafika ngazi ya Afisa Mwandamizi atakaimishwa lakini hatastahili kulipwa posho ya madaraka na badala yake atakuwa katika kipindi cha kujifunza ‘Career Develeopment’

2.3.21 Posho ya Nyumba

Iwapo una haki ya kupewa nyumba kama vile mkurugenzi au mkuu wa idara na hujapewa nyumba wala kununua nyumba ya serikali, una haki ya kupewa posho ya nyumba kwa kiwango kilichowekwa na serikali kwa mwezi (Rejea Kanuni ya L.34 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009).

2.3.22 Posho ya Sare

Iwapo wewe ni mtumishi wa kada zinazostahili kulipwa posho ya sare kama vile madaktari, wauguzi, wanasheria, makatibu mahsusi, walinzi n.k, utastahili posho hiyo kila mwaka kwa kiwango kilichowekwa na serikali.(Rejea Kanuni ya L.37 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009).

2.3.23 Posho ya Mavazi

Iwapo utapata nafasi ya kwenda nje ya nchi kikazi au kimasomo unastahili kulipwa posho ya mavazi kwa kiwango kilichowekwa na serikali. Posho hiyo italipwa mara moja ndani ya miaka miwili ili kukuwezesha kununua mavazi maalumu yanayohitajika kwenye nchi unayokwenda (Rejea Kanuni ya L.20 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009).

2.3.24 Posho za Viongozi

kiIwa utateuliwa kushika nafasi ya uongozi katika taasisi kama vile ukuu wa idara, kitengo au  ukurugenzi utastahili posho ya simu, umeme na samani kwa kuzingatia viwango vinavyotolewa na serikali kwa mwezi.

2.3.25   Kuacha Kazi

Una haki ya kuacha kazi kwa kutoa taarifa ya maandishi ya miezi 3 ya kusudio hilo au kutoa taarifa ya saa 24 ya kuacha kazi na kulipa mshahara wa mwezi husika (Rejea Kanuni ya F.49 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, 2009).

Angalizo


Kwa kuzingatia Waraka wa Katibu Mkuu UTUMISHI Kumbukumbu Na. CAC.45/257/01/D/140 wa tarehe 30 Novemba, 2010 iwapo utaacha kazi utapaswa kupata kibali cha kuajiriwa upya serikalini kama utaamua kuomba tena ajira serikalini.

 

2.3.26 Gharama za Mazishi

Ikitokea mtumishi amefariki au kufiwa na mwenza au mtoto wako, mwajiri atagharamia jeneza, uchimbaji wa kaburi, sanda, manukato na mapambo na usafiri kwenda kuzikwa eneo la makazi yako ya kudumu au eneo lingine lolote atakalochagua mtumishi mwenyewe (Rejea Kanuni ya Q.7(1-3) ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, 2009).

2.3.27 Mtumishi wa Umma Kugombea Nyadhifa za Kisiasa

Unaruhusiwa kugombea nyadhifa za kisiasa kama udiwani, ubunge na urais. Hata hivyo utaratibu ni kama ifuatavyo:-

  • Ukigombea nafasi ya ubunge katika jimbo la uchaguzi, ubunge wa viti maalumu, ubunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, mara baada ya Tume ya Uchaguzi kukutangaza kuwa mgombea wa ubunge, utalazimika kuacha kazi na utalipwa mafao yako.
  • Ukigombea nafasi ya udiwani katika kata mara baada ya Tume ya uchaguzi kukutangaza kuwa mgombea wa udiwani, utalazimika kuacha kazi na utalipwa mafao yako.
  • Ukiteuliwa na waziri mwenye dhamana na TAMISEMI kuwa diwani, utakuwa na hiari ya kuchukua likizo bila malipo kwa kipindi chote utakachokuwa diwani, au kuacha kazi na utalipwa mafao yako kuanzia siku utakayoteuliwa kuwa diwani.
  • Ukigombea nafasi yoyote ya uongozi katika chama cha siasa utalazimika kuacha kazi na utalipwa mafao yako.
  • Ukiteuliwa na Rais kuwa mbunge, utakuwa na hiari ya kuchukua likizo bila malipo kwa kipindi chote utakachokuwa mbunge au kuacha kazi na utalipwa mafao yako kuanzia siku utakayoteuliwa kuwa mbunge.

Rejea Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na. 01, 2015 kuhusu utaratibu wa watumishi wa umma wanaogombea nyadhifa za kisiasa.

 

2.4 Makosa na Adhabu

Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, zimeainisha mamlaka za nidhamu kwa makundi mbalimbali ya watumishi wa umma, aina ya makossa na adhabu zake. Mamlaka za nidhamu katika utumishi wa umma ni kama ifuatavyo:

  1. Rais ambaye ni mamlaka ya nidhamu ya Katibu Mkuu Kiongozi
  2. Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ni mamlaka ya nidhamu ya watumishi wote wanaoteuliwa na Rais.
  3. Katibu wa Bunge ambaye ni mamlaka ya nidhamu ya watumishi wanaofanya kazi Bungeni.
  4. Makatibu wakuu wa wizara ambao ni mamalaka za kinidhamu za watumishi wanaofanya kazi kwenye wizara mbalimbali
  5. Katibu Tawala wa Mkoa ambaye ni mamalaka ya kinidhamu ya watumishi wanaofanya kazi katika sekretarieti za mikoa
  6. Waziri mwenye dhamana ya TAMISEMI ambaye ni mamlaka ya nidhamu ya Wakurugenzi wa serikali za mitaa.
  7. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka za serikali za mitaa ambaye ni mamlaka ya nidhamu ya wakuu wa Idara/vitengo/sehemu na watumishi wengine maafisa.
  8. Katibu Kamisheni ya Huduma za Walimu ambaye ni mamlaka ya nidhamu ya walimu.
  9. Wakuu wa Idara ambao ni mamlaka ya nidhamu ya watumishi wasio maafisa (Operational Service)

2.4.1     Makosa ya Kinidhamu

Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma zimeainisha makosa katika makundi mawili. Makundi hayo ni makosa madogo madogo na makosa makubwa.

  1. Makosa Madogo Madogo

Makosa madogo madogo yanajumuisha ni kutokuwepo kazini bila ruhusa (utoro wa kuanzia siku mbili zitarekodiwa kama kosa linalojitegemea), kuondoka kazini wakati wa saa za kazi, kuchelewa kazini, kushindwa kukamilisha kazi uliyopewa, uzembe kazini kusikosababisha athari kwa mali ya Mwajiri na kutotekeleza maagizo uliyopewa.

Ukitenda moja ya makosa haya adhabu yake inaweza kuwa ni kupewa onyo la maandishi, karipio, kuzuiliwa ongezeko la mshahara la mwaka (Rejea Kanuni za 43(1-2) ikisomwa kwa pamoja na Jedwali la Kwanza, Sehemu B) ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003.

       ii.   Makosa Makubwa

Makosa makubwa yanajumuisha wizi, rushwa na matendo yanayofanya utumishi wa umma ukose hadhi yake. Pia, kutoheshimu mamlaka, utoro kazini wa kuanzia siku zinazozidi tano (5) na kuendelea, kutumia mali ya mwajiri kwa shughuli binafsi, kufanya kazi binafsi wakati wa kazi, na kushindwa kuripoti kituo kipya cha kazi. Aidha, kutoa siri za ofisi, kufanya kitendo tofauti na maslahi ya umma, ulevi kazini, uzembe mkubwa kazini, kufanya kosa lillilosababisha hasara kwa Mwajiri na kwenda kinyume na kanuni za maadili.


Ukitenda moja ya makosa haya adhabu zake ni pamoja na kufukuzwa kazi, kushushwa cheo na mshahara au kupunguziwa mshahara kwa 15% ya mshahara ghafi kwa muda wa miaka mitatu (3). Kipindi cha uchunguzi wa shauri la kinidhamu unaweza kusimamishwa kazi na kulipwa si chini ya nusu ya mshahara (Rejea Kanuni ya 42(1-2) ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003. Kama ilivyorekebishwa mwaka 2019

Kisa Mkasa


Chakubanga ni mzaliwa wa kijiji cha Kaloleni kilichopo mkoani Maendeleo. Baada ya kumaliza mafunzo yake ya ualimu vizuri anapangiwa kufanya kazi katika Halmashauri ya Mtakuja iliyoko mkoa wa Kazikazi. Anafunga safari kutoka kijijini kwao na anaenda kuripoti Mtakuja. Mara baada ya kuripoti Halmashauri ya Mtakuja, Mwajiri wake anampangia kufanya kazi katika shule ya msingi Mamboleo iliyoko kata ya Mjimwema kiasi cha umbali wa kilometa 16 kutoka makao makuu ya Halmashauri. Siku moja akiwa kazini (shuleni), mwalimu Chakubanga anashuhudia watoto wa kike wa darasa la sita wakipiga kelele na kuanza kuanguka ghafla na kupoteza fahamu.
Katika kutekeleza majukumu yake kama mwalimu wa zamu, mwalimu Chakubanga anaamua kumuita mganga wa kienyeji maarufu kijijini Mamboleo ili kuja kutoa mashetani yaliyoko eneo la shule wanaosababisha watoto kupiga kelele, kupoteza fahamu na kuanguka.
Mara baada ya mganga kufika eneo la shule na kuanza kufanya kazi yake waandishi wa habari nao wanafika na kuanza kumhoji mwalimu Chakubanga, naye bila hiyana anawaelezea waandishi husika tukio zima lilivyotokea na maamuzi aliyoyafanya.
Mganga anafanya kazi yake na anapomaliza anadai alipwe fedha sh 200,000. Mwalimu Chakubanga anachukua fedha za shule zilizochangwa na wazazi kwa ajili ya madawati anamlipa mganga na kumpa maelekezo mganga kuwa atawaeleza wazazi kuwa ametumia shs 400,000 kumlipa mganga ili na yeye abakie na hela kidogo (tsh. 200,000/=) ili ampe mwanafunzi Asha wa darasa la 7 aende hospitali ili atoe  ujauzito aliompatia.
Siku ya kikao cha wazazi Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mamboleo anatoa taarifa kwa wazazi juu ya tukio la wanafunzi kuanguka. Anamlaumu mwalimu Chakubanga wazi wazi mbele ya wazazi kuwa hakumshirikisha katika kumwita mganga wa kienyeji. Pia, anawatangazia wazazi kuwa anamsimamisha kazi mara moja mwalimu husika kwa kosa la kutumia fedha za madawati kumlipa mganga bila ridhaa yake. Wazazi wanapotaka kutoa maoni yao, mwalimu mkuu anawazuia na kueleza zaidi kuwa anamtaka mwalimu Chakubanga alipe fedha husika ndani ya siku 5 la sivyo atamfukuza kazi na kisha anafunga kikao.
Mwalimu Chakubanga baada ya kuona mambo magumu anaamua kutoroka usiku bila ya kuaga na kurudi kijijini kwao Kaloleni.
Maswali:
  1. Taja makosa aliyoyatenda mwalimu Chakubanga.
  2. Taja makosa aliyoyatenda mwalimu mkuu.
  3. Ni hatua gani sahihi ambazo mwalimu Chakubanga alipaswa kuzifuata kutatua matatizo yaliyojitokeza?
  4. Ni utaratibu gani sahihi mwalimu mkuu alipaswa kuufuata ili kumchukulia hatua stahiki mwalimu Chakubanga?

Matangazo

  • Wanafunzi waliochaguliwa Shule za Vipaji maalumu,Ufundi,Bweni kawaida na shule maalumu 2023 December 14, 2022
  • wavulana waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2023 simanjiro day schools December 14, 2022
  • wasichana waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2023 Wilaya ya Simanjiro day schools December 14, 2022
  • Tangazo la Ajira Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro May 23, 2022
  • Ona vyote

Habari Mpya

  • Nyerere day

    October 14, 2024
  • Mkutano wa wadau kuhusu utoaji wa maoni ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050

    July 29, 2024
  • MWENGE WA UHURU

    July 16, 2024
  • Kifo Cha Raisi awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi 2024

    February 29, 2024
  • Ona vyote

Video

Mh.Dr Serera azindua kipindi cha Pili awamu ya Tatu ya TASAF Wilayani Simanjiro
video Zaidi

Fika kwa Haraka

  • Government Mailing System
  • Mission and Vision
  • Organization Structure
  • Completed Projects

Kiungo Muunganisho

  • Ikulu
  • Utumishi
  • Matokeo kidato cha sita 2021
  • TAMISEMI
  • Ofisi ya Taifa ya Takwimu
  • Idara ya Habari-Maelezo

World visitors tracker

world map hits counter

Visitors Counter

free HitCounter

Ramani ya Mahali

Wasiliana Nasi

Other Contacts

   

    • Government Mailing System

copyright@2016 Halmashauri ya Wilaya Simanjiro.Haki zote zimehifadhiwa