Wilaya ya Simanjiro ni kati ya Wilaya tano (5) zinazounda Mkoa wa Manyara. Wilaya ilianzishwa mwaka 1993 ikimegwa kutoka wilaya ya Kiteto. Wilaya inapakana na wilaya ya Monduli upande wa Kaskazini Magharibi, wilaya za Arumeru, Hai na Moshi upande wa kaskazini, Kiteto upande wa kusini, Kondoa na Babati upande wa Magharibi na Mwanga, Same, Kilindi na Korogwe upande wa Mashariki. Wilaya ina eneo lenye jumla ya kilometa za mraba 20,591
Wilaya iko katika eneo la nyanda kame na mbuga, hivyo hupata mvua za wastani wa kati ya milimita 400 na 500 kwa mwaka. Wilaya ina vipindi viwili vya mvua ambavyo ni vuli na masika. Mvua za vuli hunyesha kuanzia mwezi Novemba hadi Desemba na masika hunyesha kuanzia mwezi Machi hadi Mei.
Wilaya ya Simanjiro ina Tarafa sita (6), Kata kumi na nane (18), Vijiji hamsini na saba (57) na Vitongoji mia mbili themanini na moja (281). Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Wilaya ilikuwa na jumla ya wakazi 178,693, kati yao Wanawake ni 89,718 na Wanaume 88,975.Kwa mwaka 2018 Wilaya inakadiriwa kuwa na jumla ya wakazi 219,131, kati yao wanawake 111,757 na wanaume 107,374 sawa na ongezeko la asilimia 3.2 kwa mwaka.
Hali ya ulinzi na usalama katika Wilaya ya Simanjiro ni ya kuridhisha kwani hakuna matukio makubwa ya kutisha isipokuwa uhalifu mdogo mdogo unaodhibitiwa na vyombo vya ulinzi na usalama. Mahusiano ya vyombo vya ulinzi na usalama,taasisi za serikali, vyombo vya utawala na uwakilishi wa wananchi,taasisi za kidini, mashirika ya umma na binafsi ni ya kuridhisha.Serikali ya wilaya imeendelea kusimamia mamlaka za Vijiji, Kata na Tarafa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.
Kunapokuwepo na viashiria vya migogoro hushughulikiwa mapema na mamlaka ya Wilaya na kupatiwa ufumbuzi stahiki. Wilaya haina migogoro ya kidini, kisiasa wala ukabila.
1.5 HALI YA SIASA NA UTAWALA NA JINSI MALALAMIKO /KERO MBALIMBALI ZINAVYOSHUGHULIKIWA
Hali ya kisiasa ipo salama katika eneo lote la Wilaya na hakuna tukio lolote baya lililoripotiwa. Aidha vyama mbalimbali vya siasa vinafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Kwa upande wa Malalamiko na kero, Wilaya ina utaratibu wa kutatua kero na malalamiko kwa njia mbalimbali zikiwemo mikutano ya hadhara, vikao mbalimbali katika ngazi za vijiji, kata mpaka Wilaya. Pia Wilaya imeanzisha madawati ya malalamiko katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji ambayo hushughulikia kero na malalamiko kutoka kwa jamii. Katika kipindi cha Januari hadi Aprili 2018 jumla ya kero 110 za watu binafsi zimepokelewa na kutafutiwa ufumbuzi kupitia madawati haya na migogoro ya mipaka 9 ilifanyiwa kazi na migogoro 2 inayohusisha ugomvi wa kijamii ilitatuliwa pia.
Halmashauri ya Wilaya Simanjiro Bomani street-Orkesumet
Sanduku la Posta: P.o Box 9596,Orkesumet,Simanjiro,Manyara,Tanzania
Simu: Tel:027-29707889
Simu: +255-758350936
Barua pepe: ded@simanjirodc.go.tz
copyright@2016 Halmashauri ya Wilaya Simanjiro.Haki zote zimehifadhiwa